Umeshawahi kula nyama ya bata? Iwe ni rosti,ya kukaanga au ya kuoka au kavu bila shaka ulifurahia ladha adimu ya kitoweo hicho.
Wakati wengine wakifurahia utamu wa nyama hiyo, wapo ambao hawaipendi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo baadhi ya wapishi kushindwa kuiandaa inavyotakiwa.
JikoPoint imekusogezea namna bora ya kuandaa nyama ya bata ili uweze kufurahia labda adimu ya kitoweo hicho huku ukijpatia faida nyingine nyingi za kiafya.
Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) imezitaja faida za kutumia nyama hiyo kuwa ni chanzo kizuri cha virutubisho ambavyo ni muhimu kwa afya na ukuaji kwa ujumla.
Bila kupoteza muda tuingie jikoni kuandaa kitoweo hiki kinachoweza kunogesha kifungua kinywa, mlo wa mchana hata ule wa usiku.
Tupike pamoja
Hatua ya kwanza baada ya kuchinja bata ni kuchemsha maji kwa ajili ya kunyonyoa manyoya yote yaliyopo katika nyama ya bata kisha utaendelea kwa kutaka nyama katika vipande vitakavyoendana na mahitaji yako.
Usisahau kuosha vipande vyako vya nyama kwa maji safi kabla ya kuendelea na hatua nyingine, hakikisha umeondoa uchafu wote unaoweza kuwepo ndani na nje ya vipande vya nyama.
Ili kuepusha harufu ya shombo ya nyama ya bata ambayo walaji wengi hawaipendi ni vyema kuloweka vipande vya nyama ya bata kwenye mchanganyiko wa maji na limao kwa muda wa dakika 30 ili kuondoa harufu.
Baada ya hapo katika blenda saga vitunguu maji, vitunguu saumu, tangawizi, mdalasini, karafuu, na pilipili manga hadi viwe laini, ila ikitokea huna blenda unaweza kutumia kinu cha kawaida kusaga mchanganyiko huo.
Hatua inayofuata weka vipande vya bata kwenye sufuria ongeza mchanganyiko wa viungo ulivyosaga kisha koroga vizuri ili viungo vikolee katika nyama.
Washa jiko bandika mafuta kwenye sufuria kubwa ama kikaango cha kukangia pia unaweza tumia oveni au “airflyer’ kama unayo ili kumkaanga bata vizuri.
Unaweza pia kuanza kwa kuchemsha nyama ya bata kwa dakika 30 mpaka 40 kwa moto wa wastani ndipo uendelee na hatua ya kukaanga ili kuepuka kutumia mafuta mengi.
Kaanga hadi nyama ibadilike na kuwa na rangi ya kahawia na hapo itakuwa tayari kwa matumizi mengine ikiwemo kuunga mchuzi au kutumiwa pamoja na wali, ugali, au chapati.
Kama utataka kuiunga basi kaanga kitunguu kikiiva weka nyanya na viungo vingine kama pilipili hoho, karoti kisha uache ziive na kuwa rojo nzito ongeza supu ya nyama ya bata uliyobakisha mwanzoni, viungo vya mchuzi na kisha uweke nyama uliyoikaanga na ikichemka rosti yako itakuwa tayari kwa kula
Furahia mlo wako, ila usisahau kuendelea kutembelea tovuti ya Jiko Point ili kufurahia mapishi mbalimbali.