Je umeshawahi kula kachori za mbogamboga? Kama bado leo nitakupa maujanja.
Baadhi ya watu wamezoea kachori lazima ziwe zimepikwa kwa viazi mviringo (viazi mbatata), mihogo au viazi vitamu jambo ambalo limekuwa ni kawaida katika jamii za Afrika.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) utumiaji wa mbogamboga katika kila mlo husaidia kuzuia na kukabiliana na saratani na kuimarisha mfumo wa kingamwili na kukuepusha na magonjwa.
Hivyo leo ndani ya jikopoint.co.tz unajifunza njia mpya ya kupika kachori kwa kutumia mchanganyiko wa mbogamboga ambazo sio tu zina ladha tofauti lakini pia zina faida nyingi kiafya.
Hatua kwa hatua namna ya kuandaa
Hatua ya kwanza, chukua karoti, hoho, kabichi na vitunguu safisha kwa maji safi ili kuondoa uchafu na wadudu. Kisha zimenye na kuzikata katika vipande vyembamba na virefu. Pia katakaka kabichi.
Baada ya hapo weka maji motoni katika sufuria yako na yaache yachemke kwa dakika 3 kisha weka mchanganyiko huo hapo juu na uongeze chumvi kiasi.
Geuza kwa dakika 2 usiache vichemke kwa muda mrefu. Baada ya hapo epua kutoka katika sufuri lenye maji ya moto kiasi na uwekwe kwenye chombo chenye maji ya baridi kwa lengo la kupoza mboga mboga.
Mboga ikipoa chuja kwa chujio ili kuondoa maji katika mchanganyiko wako. Katika bakuli lingine weka unga wa ngano robo kilo, pilipili (kama unapenda ila sio lazima), majani ya kotimiri kiasi kisha ongeza mbogamboga na uchanganye mchanganyiko huo mpaka ushikane vizuri na unga.
Baada ya hapo tengeneza madonge madogo mfano wa mpira. Hatua inayofuata weka mafuta ya kutosha kwenye kikaango.
Mafuta yakipata moto, weka kachori moja baada ya nyingine na kaanga mpaka ziwe na rangi inayovutia. Hakikisha moto usiwe mkali sana ili ziive vizuri.
Kufikia hatua hiyo kachori zako za mboga mboga zitakuwa tayari kwa kuliwa na unaweza kula na juisi, soda, chai ama zenyewe ni wewe tu upendavyo.