Njia rahisi za kupika mkate nyumbani

Na Lucy Samson
23 Jan 2023
Jifunze kuandaa mkate nyumbani kwa kutumia jiko la mkaa, na upunguze gharama kubwa uliyokuwa unaitumia kununua kitafunwa hicho.
article
  • Ni rahisi kuaanda mkate huu ukiwa nyumbani.
  • Hakuna haja ya kutumia oven, jiko la mkaa lina uwezo mkubwa wa kuivisha pishi hili
  • Hupunguza gharama za vitafunwa kwa familia yenye watu wengi

Mkate ni moja kati ya kitafunwa maarufu kinachotumika kwenye kifungua kinywa wakati wa asubuhi, huku kikisindikizwa na chai, juisi au soda.

Wakati huu ambao wanafunzi wamefungua shule, mkate ndio kitafunwa rahisi kinachopatikana kwa haraka mtaani na kuwezesha familia kupata kifungua kinywaji asubuhi.

Hata hivyo, kwa familia yenye watoto wengi wanaoenda shule wakati wa asubuhi ununuzi wa kitafunwa hiki unaweza kuwafanya wazazi au walezi kutoboa mifuko yao zaidi ili kuwezesha upatikanaji wake.

Usilolijua ni kwamba unaweza kuandaa vitafunwa nyumbani kwa kutumia jiko la mkaa, na ukapunguza gharama kubwa uliyokuwa unaitumia kununua kitafunwa hicho.

Makala hii imekuandalia hatua rahisi za kupika mkate kwa kutumia jiko la mkaa.

Maandalizi

Hatua ya kwanza katika mapishi haya ya mkate, ni kuandaa unga wa ngano kwa kuuchekecha na kutoa uchafu wote unaoweza kuwepo.

Katika hatua hii unaweza kutumia chujio la chai, kama hauna unaweza kutumia mikono kutoa uchafu wote unaoonekana.

Baada ya hapo changanya unga wa ngano, hamira, sukari, sukari na kiasi cha maji na ukande mpaka unga uwe laini.

Ukandaji huu ni sawa na ule wa kukanda unga wa maandazi au chapati, hakikisha tu unga umelainika vizuri na uuache uumuke kwa saa moja.

Faida ya kupika mkate wako mwenyewe ni uwezo wa kuchagua umbo na ladha uipendayo. Picha | Shuna’s Kitchen.

Baada ya saa moja funua na kanda tena kisha andaa chombo cha kuokea kwa kukipaka mafuta kisha uweke unga na uuache kwa nusu saa au zaidi  uumuke tena.

Wakati unasubiri unga uumuke washa jiko la mkaa na uache likolee vizuri, kisha tafuta sufuria kubwa utakayoitumia kuchoma mkate wako.

Lengo la kutumia sufuria kubwa ni kuzuia moto usipitilize moja kwa moja na kuunguza mkate wako kwenye chombo cha kuchomea ulichoweka.

Katika hatua hii, kuna baadhi ya watu wanatanguliza kiasi kidogo cha mchanga kisha kufufuatiwa na sufuria ya kuokea kama inavyoonekana hapo chini.

Wengine wanaweka moja kwa moja chombo cha kuokea juu ya sufuria kubwa huku wakiwa makini na kiwango cha moto walichokibakisha jikoni.

Baada ya kubandika jikoni funika na upalie moto wa wastani kisha uache uive kwa nusu saa mpaka dakika 45.

Muda huo ukipita unaweza kuangalia mkate wako kama umeiva epua na uache upoe kwa dakika tano kabla ya kupeleka mezani au kuukata saizi uipendayo.

Mpaka hapo  mkate wako upo tayari kuliwa.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa