Kwa kawaida kwenye siku ya wapendao tumezoea kuwatoa ‘out’ wenza wetu ili wakapate chakula cha tofauti na kile wanachokula mara kwa mara .
Wengine tumekuwa tukiwapeleka kwenye migahawa maarufu, na kwa wale wenye ‘mapene’ zaidi, basi siku hiyo chakula cha hotel zenye hadhi huusika.
Lakini unatambua kuwa unaweza kumuandalia mwenyewe mpenzi wako chakula special nyumbani?
Binafsi hii naona imekaa kimahaba zaidi.
Moja ya pishi ambalo unaweza kuandaa kwa ajili ya siku hii, ni pamoja na “chicken balls”, jina lisikutishe, pishi hili ni rahisi sana kuandaa.
Tuanze maandalizi
Cha kwanza kabisa saga nyama kwenye mashine ya kusagia nyama. Tafadhali! usije weka maji. Kama hauna mashine hiyo, unaweza kununua nyama ya kuku iliyosagwa moja kwa moja buchani.
Nyama itakaposagika, anza kuweka viungo, yaani pilipili manga, tangawizi ya unga, kitunguu swaumu cha unga, masala ya kuku, pili pili ya unga (sio lazima) pamoja na chumvi.
Pia kama hauna blenda, unaweza kuchanganya kawaida.
Changanya vizuri mchanganyiko huo, kisha paka mafuta ya kupikia kwenye mikono yako, kama vile huwa tunafanya wakati wa kumenya ndizi mbichi.
Anza kutengeneza matonge ya nyama kwa saizi uipendayo lakini usitengeneze makubwa sana.
Hatua inayofata, utachukua manda za sambusa na ili kuokoa muda tumia zile ambazo zimeshatengenezwa kabisa. Manda hizi unaweza kuzipata supermarket kuanzia Sh2500.
Tenganisha manda kwa kuzibandua kwa sababu zinakuwa zimegandana, bandua kiasi ambacho kitatosha idadi ya matonge ya nyama uliyotengeneza.
Kisha katakata manda katika vipande vidogo vidogo. Baada ya hapo chukua tonge moja moja na uviringishe kwenye manda ulizokata kata.
Hadi hapo chicken balls zako zinakuwa tayari kukaangwa.
Makaangizo
Weka mafuta kwenye kikaango ambayo yatatosha kukaanga vizuri ‘chicken balls’, usiweke mafuta mengi sana.
Kama una mashine ya kukaangia vitu yaani “deep fryer” itakuwa bomba zaidi lakini kama hauna, sufuria lako kwenye jiko la gesi au ummee litafanya poa.
Mafuta yatakapochemka kidogo anza kukaanga chicken balls, hakikisha moto ni wa wastani ili usije babua au kuunguza pishi lako.
Kaanga chicken balls hadi zitakapoanza kupata rangi ya kahawia, hadi hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.
Unaweza kaanga chipsi au ndizi ili kusindikizia pishi lako bila kusahau kinywaji ukipendacho cha kushushia.
Si umeona ilivyo rahisi? Haya sasa ni wakati wako wa kuonesha mahaba kwa umpendae na kuokoa gharama za kununua chakula.
Usisahau kuandaa vizuri meza yako ya chakula,walau kwa maua na mishumaa kidogo ili dinner yenu iwe ya kuvutia.