Unga wa ngano una aina nyingi za mapishi. Achana na maandazi, chapati za maji, kalmati, mikate na chapati za kusukuma za kawaida unazokula kila siku.
Leo tujifunze kupika chapati za kusukuma zenye nyama ya kusaga.
Pishi hili mbali ya kunogesha mlo wa asubuhi, mchana au jioni linaweza pia kutumika kibiashara na likakuongezea wateja na kipato chako kikaongezeka pia.
Fuatana nami mpaka mwisho wa makala hii ujifunze, uongeze ujuzi kisha uhamishie nyumbani kwako au kwenye mgahawa wako.
Maandalizi
Hatua ya kwanza ni kuandaa nyama ya kusaga kwa kuiosha na kuikausha maji.
Osha hoho, karoti na kitunguu maji na ukate kate kwa saizi unayoipenda, kisha weka kwenye chombo kisafi kwa ajili ya kuvitumia wakati wa kuandaa chapati yako yenye nyama ndani.
Baada ya maandalizi sasa tuanze kwa kupika nyama ya kusaga itakayochanganywa na ngano ili kutengeneza chapati yenye nyama ndani.
Bandika sufuria jikoni ongeza mafuta kiasi yakipata moto weka vitunguu maji, koroga mpaka viwe rangi ya kahawia.
Ongeza kitunguu swaumu kilichosagwa na ukoroge kwa dakika moja kisha weka nyama ya kusaga ikoroge vizuri kisha ufunike ichemke mpaka maji yaliyopo yakauke.
Nyama yako ikikauka maji ongeza chumvi, pilipili manga kijiko kimoja, masala kijiko kimoja na ukoroge vizuri. Ongeza pilipili hoho na karoti, funika kwa dakika tano kisha nyama yako itakuwa tayari.
Tukishaandaa nyama ya kusaga sasa tuandae chapati kwa kuanza kuchekecha unga wa ngano ili kuondoa mabonge bonge ya unga na kuhakikisha unga wetu ni msafi.
Ukishahakikisha unga wako ni msafi andaa bakuli la kukandia kisha weka unga, ongeza chumvi robo kijiko, na mafuta kiasi au siagi ya kukandia. Ongeza na maji kiasi kisha uanze kukanda.
Kanda unga wa chapati kwa dakika 15 au zaidi kwa kutegemea wingi wa unga.
Unga ukilainika ongeza mafuta ya kupikia vijiko viwili au siagi kisha ukande tena kwa dakika 3 ili unga uchanganyike vizuri na mafuta.
Ugawe kwa kuukata madonge matano au sita kulingana na wingi wa unga wako na ufunike kwa dakika 10 au zaidi kabla ya kusukuma.
Baada ya dakika 10, chukua donge moja moja na usukume kutengeneza duara kisha weka nyama ya kusaga kiasi katikati na ulifunge duara kwa kulizungusha.
Rudia hatua hiyo kwa madonge mengine yaliyobakia kisha uanze kusukuma madonge uliyokwisha kuyafunga na nyama ndani.
Sukuma donge lako vizuri kupata chapati yenye muonekano mzuri, wengine hutengeneza chapati yenye pembe nne siyo lazima duara.
Ukisha sukuma vizuri washa jiko, andaaa kikaangio kwa ajili ya kuchoma chapati zako mpaka ziive vizuri.
Rudia hatua hiyo kwenye maduara mengine yaliyobaki na chapati yako itakuwa tayari