Unavyoweza kupika wali usio na mboga 

Na Lucy Samson
21 Jul 2022
Katika pishi hili utahitaji  mchele, mafuta ya kupikia, kitunguu maji na swaumu na nyanya.
article

  • Mahitaji ni mchele, kitunguu maji na swaumu.
  • Pia mafuta, sufuria na jiko la gesi.
  • Wali huu unaweza kula bila mboga yoyote.

Mimi huwa sipiki mara kwa mara, ila leo nikaona acha nijaribu kupika, nikawaza nipike chakula gani cha  haraka haraka maana nilikuwa na njaa, alafu muda ulikuwa umeenda sana.

Kwa haraka nikaanza kuangalia nina nini ndani, macho yangu yalitua kwenye madebe tupu ya unga na mchele uliobaki kidogo kwenye moja ya madeli. Nikaamua kupika wali.

Sauti nyingine ikanijia kichwani nitapika wali na nini? Nikajijibu kuwa nitapika wali usio na mboga huku nikitabasabu nilianza kuandaa pishi hili ambalo ni rahisi na halina mahitaji mengi.

Mahitaji ya wali usio na mboga ni matano  tu ambayo hayawezi kukugharimu zaidi ya Sh3,000

Katika pishi hili utahitaji  mchele wenyewe, ambao mimi nilikuwa nao ndani, ila  unaweza ukanunua  mchele nusu kwa Sh1,000, mafuta ya kupikia ya Sh500, kitunguu swaumu cha 200 nyanya na kitunguu cha 100.

Twende jikoni sasa kwa ajili ya kuandaa wali usio na mboga. Pishi hili linachukua dakika 20 tu kama utatumia jiko la gesi.

Tuanze kwa kuchambua mchele na kuuosha, kisha menya kitunguu swaumu na ukitwange mpaka kilainike. Menya nyanya na kitunguu ukikate kate kwa saizi ya duara.

Washa jiko, chemsha maji kwa ajili ya kupika wali wako, kisha ubandike sufuria nyingine, uweke mafuta kiasi kwa ajili ya kuanza mapishi ya wali huu wenye ladha ya kipekee.

Mafuta yakichemka weka kitunguu swaumu ukikaange, baada ya dakika mbili ongeza kitunguu maji na ukoroge mpaka kiwe rangi ya kahawia. Ongeza nyanya na ufunike ziive.

Nyanya zikiiva ongeza maji ya moto uliyoyachemsha na chumvi kisha uweke mchele na uache uive kwa moto mdogo.

Mimi leo nimetumia jiko la gesi hivyo hakuna masuala ya kupalia baada ya dakika 20 nitageuza wali wangu na kusubiri kwa dakika tano zaidi ili uive vizuri.

Wali sasa uko tayari, hauna haja ya mboga hivyo unaweza kutafuta juisi ya matunda, ili kushushia.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa