Mambo ya kufanya unapohisi gesi imevuja nyumbani

Na Mariam John
5 Aug 2022
Unashauriwa kutowasha taa, kufungua friji, asiwashe kiberiti na anatakiwa kufungua madirisha ili kuruhusu hewa safi kuingia ndani ya nyumba.
article
  • Fungua madirisha na milango kuruhusu hewa kuingia ndani.
  • Usiwashe taa au friji unapohisi gesi inavuja.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetoa tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa kwa mtumiaji wa gesi ya majumbani (LPG) pale wanapohisi inavuja ikiwemo kufungua madirisha na milango kuruhusu hewa iingie ndani.

Akizungumza Nukta habari (www.nukta.co.tz) kwenye maonyesho ya Nane Nane yanayofanyika nje kidogo ya jiji la Mwanza katika viwanja vya Nyamhongolo, Meneja wa Ewura Kanda ya Ziwa, George Mhina amesema pamoja na kwamba Serikali inahamasisha matumizi ya nishati hiyo ya kupikia lakini watumiaji wanapaswa kuwa waangalifu pale wanapohisi kuna kihitarishi kinachosababishwa na gesi hiyo.

Mhina ameainisha mambo muhimu manne yanayopaswa kuzingatiwa iwapo mtumiaji atahisi kuna harufu ya gesi au gesi inavuja ndani ya nyumba yake. Mojawapo ni kutowasha taa kwa kuwa zipo taa ambazo zinaweza kusababisha cheche na kusababisha mlipuko.

Pia mtumiaji hapaswi kufungua jokofu au friji, asiwashe kiberiti na anatakiwa kufungua madirisha ili kuruhusu hewa safi kuingia nadani ya nyumba.

“ Tunaendelea kutoa elimu hii kwa kuwa hivi sasa Serikali imeanza kuhamasisha matumizi ya gesi hadi vijijini, hivyo ili kuepuka matatizo yanayoweza kusababishwa na gesi kuvuja  jamii inatakiwa kujua mbinu hizo muhimu,” amesema Mhina. 

Meneja huyo pia ametumia fursa hiyo kuwataka wauzaji wa mitungi ya gesi kuacha uchakachuaji wa gesi na atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.

Mhina amewataka watumiaji pale wanapoenda kununua gesi kuhakikisha wanaipima ili kuona ujazo wa gesi kama uko sawa kulingana na kiwango alichoenda kununua lakini pia kuangalia lakiri.

“Pia tunawaasa watumiaji wanaposafirisha gesi wahakikishe wanaiacha angalau kwa muda wa dakika tano ndipo aanze kuitumia,” amesema Mhina.

Hata hivyo amesema hivi sasa Serikali inapambana kuhakikisha wananchi wanatumia nishati mbadala ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Anasema mbali na uharibifu wa mazingira lakini pia nishati hiyo ya kuni na mkaa inasababisha magonjwa ya ngozi na macho na wakati mwingine akina mama kuitwa wachawi.

“Kiuhalisia mtu anayetumia kilo sita za mkaa kwa siku angetumia gesi angetumia kilo moja hivyo badala ya kutumia Sh2,000 kununulia mkaa na kuni kila siku angenunua gesi angeweza kutumia kilo sita tu kwa mwezi,” amesema Mhina.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa