Tangsen yachagiza matumizi ya nishati safi ya kupikia Pwani

Na Daniel Samson
17 Feb 2025
Yawakutanisha wadau wa nishati kujadili mikakati ya kuendeleza nishati safi na salama ya kupikia wilayani Kisarawe mkoani Pwani
article
  • Ni pamoja na elimu na kujumuisha makundi yote kwenye jamii.
  • Ajenda ya nishati safi yahimizwa kuwa sehemu ya mipango ya halmashauri.

Dar es Salaam. Wananchi mkoani Pwani wameshauriwa kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia huku wadau wa nishati wakipendekeza mabadiliko ya sheria na uboreshaji wa mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame ili kuokoa mazingira mkoani humo. 

Afisa Maliasili Mkoa wa Pwani, Pierre Protas amesema Serikali ya Mkoa wa Pwani imekuwa ikishirikiana na taasisi binafsi kuelimisha wananchi na kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuhimiza matumizi ya nishati safi ili kuokoa mazingira. 

“Binadamu tunazidi kuongezeka, ardhi na rasilimali ni zile zile, tunasisitiiza kubadilisha nishati za kuni na mkaa na kuanza kutumia teknolojia zinazopunguza nishati hizo lakini kutumia nishati nyingine mbadala ili tuokoe mazingira kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Protas. 

Protas alikuwa akizungumza katika warsha kuhusu kujumuisha mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (CCAPs) katika mipango ya maendeleo ya wilaya (DDPs) kwa kuzingatia jinsia katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe iliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia na Nishati Endelevu Tanzania (Tangsen) Februari 14, 2025.

Protas amesema ikiwa wananchi wa Pwani wataongeza kasi ya kutumia nishati safi watakuwa wanatekeleza malengo ya Serikali ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi na salama ya kupikia ifikapo mwaka 2034. 

Afisa Maliasili Mkoa wa Pwani, Pierre Protas (Aliyesimama) amesema matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia ni njia mojawapo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Picha | Tangsen.

Tangsen imekuwa ikitekeleza mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuzingatia jinsia katika wilaya tatu za Mkoa wa Pwani: Rufiji, Kibaha na Kisawarawe tangu mwaka 2019. 

Makundi mbalimbali wakiwemo viongozi na wanawake wamekuwa wakielimishwa na kufundishwa namna ya kuanzisha miradi inayotumia nishati safi na teknolojia iliyoboreshwa ili kutengeneza ajira, kipato na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame. 

Mratibu  wa Miradi kutoka Tangsen, Leonard Pesambili aliyekuwa akizungumza katika warsha hiyo amesema makundi yaliyopo kwenye jamii yafikiwe na kupewa elimu ya nishati safi ya kupikia kulingana na mahitaji yao. 

“Tuwawezeshe vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupata teknolojia na mitaji ya kuwekeza katika biashara za nishati safi,” amesema Pesambili. 

Pesambili amesema ushiriki wa viongozi wa Serikali wakiwemo wenyeviti wa vijiji, madiwani katika utekelezaji wa mipango ya matumizi ya nishati ni muhimu kwa sababu wana ushawishi kwenye jamii. 

“Viongozi kama madiwani wawe mstari wa mbele kutumia nishati na iwe ajenda ya kisiasa na maendeleo na wawe mabalozi wa kutumia nishati hiyo katika maeneo yao,” amesema Pesambili. 

Mratibu  wa Miradi kutoka Tangsen, Leonard Pesambili (aliyesimama) amesema elimu na teknolojia ya kisasa inaweza kusaidia kuchagiza matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia. Picha | Tangsen.

Mtaalam huyo wa nishati na mazingira anasema Tangasen itaendelea kushirikiana na makundi yote kwenye jamii wakiwemo viongozi kutekeleza CCAPS ili kuhakikisha unajumuishwa katika mipango ya halmashauri ili kurahisisha utekelezaji wake. 

Hatua za kufuata ili kuunda CCAPS ni pamoja na kuainisha maeneo ambayo yanathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, kufanya utafiti upembezi yakinifu na kuwasilisha matokeo kwa wadau wakiwemo viongozi na mwisho kuandaa mkakati wenye malengo, muda wa utekelezaji, bajeti na rasilimali ya kutekeleza shughuli zilizopangwa.

Naye Revocatus Samwel, muongozaji katika warsha hiyo amesema utashi wa kisiasa kuhusu nishati safi na salama ya kupikia ni muhimu ukaenda na sambamba na uboreshaji sheria zinazosimamia mazingira na nishati ili kupunguza mgongano ambao umekuwa ukipunguza kasi ya kuhamia katika matumizi ya nishati safi.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa