Dar es Salaam. Huenda tatizo la kukatika kwa umeme likamalizika nchini mara baada ya kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) kuanza utekelezaji wa miradi mitano ya kipaumbele ya rasilimali ya jotoardhi itakayoongeza upatikanaji wa nishati hiyo nchini.
Kampuni hiyo ni kampuni tanzu ya Shirika la umeme Tanesco ambapo inatekeleza nishati ya jotoardhi inayochimbwa urefu wa kilometa tatu kwenda chini na ambapo rasilimali zilizopo zinaweza kuzalisha umeme wa megawati 5,000.
Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni ya TGDC, Mhandisi Shakiru Kajugus alikuwa akizungumza hivi karibuni katika ziara ya Bodi ya Wakurugenzi ya kampuni hiyo ilipotembelea eneo la mradi lililipo Ziwa Natron wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.
Amesema kuwa, nishati hiyo ya jotoardhi inapatikana kwa wingi katika maeneo ya bonde la ufa ambapo kwa upande wa Ziwa Natron wapo katika hatua za utafiti kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ambao utazalisha megawati 60 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2025 .
“Mradi huu wa Ziwa Natron kwa kuanzia tutazalisha megawati 10 baada ya hapo tunaendelea na upanuzi zaidi na unatarajiwa kugharimu kiasi cha zaidi ya Sh1 bilioni na kukamilika kwa mradi huo kutaleta manufaa makubwa sana kwa wananchi kwani ni nishati endelevu ya kisasa isiyotegemea mabadiliko ya tabianchi,” amesema Mhandisi Kajugus.
Tanzania kwa sasa inatekeleza miradi mitano ya kipaumbele ya joto ardhi ikiwemo Wilaya ya Rungwe katika maeneo ya Ngozi na Kiejo – Mbaka mkoani Mbeya.
Mikoa mingine ni Songwe na Pwani na tayari ipo katika hatua ya uhakiki kwa ajili ya kuchimba visima huku kwa mkoa wa Arusha wakiendelea na tafiti za kisayansi ambazo zinatarajiwa kumalizika mwaka 2023.
Nishati ya jotoardhi ina matumizi mengi ikiwemo kuzalisha umeme ambao hutumika kuendeshea mitambo, kupikia na kutoa mwanga majumbani.
Mwenyekiti wa bodi ya TGDC, Profesa Shubi Kaijage amesema bodi mpya wamefikia hatua ya kutembelea moja ya miradi ya jotoardhi kujionea na kuweza kuangalia cha kushauri ili mradi huo uweze kufanyiwa kazi kwa haraka na kwa weledi.
Amesema kuwa, nishati hiyo inapatikana chini ya ardhi kwa kutumia joto lililopo chini ya ardhi na kuwa itaweza kupunguza changamoto ya mgao wa umeme uliopo hivi sasa unaosababishwa na ukame.
“Sisi kama bodi tunaendelea kuhakikisha tunasimamia kikamilifu mradi huu ili uweze kukamilika kwa wakati na tunaomba kampuni hii iendelee kutekeleza majukumu yake kwa wakati ili tuendelee kupata vyanzo zaidi vya umeme,” amesema Prof Kaijage.