Dar es Salaam. Kwa wazee baba huenda kati ya vyakula vigumu kupika ikawa ni vyakula vya vitafunwa.
Nazungumzia mkate, maandazi, chapati na hata keki.
Kwa ambao huenda mbali, labda huchemsha viazi na mihogo au magimbi lakini kinachohusisha unga wa ngano, wachache wamefanikiwa kuuvuka mstari huo wa upishi.
Leo, nakusogezea pishi simpo kabisa na huenda likawa ni pishi lako pendwa baada ya kujifunza kulipika. Ni chapati.
Usiogope sasa, siyo za kusukuma, ni chapati za maji.
Kwa sababu wanaume wengi hawapendi kukaa jikoni kwa muda mrefu, leo kitafunwa hiki kitakuwa rahisi kuandaa.
Licha ya kuwa ni rahisi kiuandaaji, inahitaji kuzingatia baadhi ya mambo muhimu ili usije kutoa ‘boko’.
Mambo hayo ni pamoja na mahitaji muhimu kwa ajili ya kitafunwa hiki ikiwemo maiwa na maji.
Tuandae uji wa chapati
Cha kuanza ni kuweka unga wako kwenye bakuli kubwa ili kupata urahisi wa uaandaaji, kisha anza kuongeza maziwa yako na kama hauna maziwa, unaweza kutumia maji.
Koroga mchanganyiko wako uhakikishe uji wako hauna mabonge ya unga. Unaweza kutumia “haand mixer ya umeme kama unayo kama hauna, hakuna kilichoharibika.
Hakikisha unapatz uji mzito kiasi, kwa uelewa, unaweza kuilinganisha na uzito wa juisi ya embe.
Baada ya hapo, ongeza mayai sukari na chumvi kisha ukoroge hadi vitakapo yeyuka vizuri kwenye uji wako, hadi hapo mchanganyiko wako utakua tayari.
Kwa ambao hawapendi sukari, unaweza kuweka chumvi na wasiopenda chumvi wanaweza kuweka sukari ili kupata ladha.
Unaweza kuongezea madiko diko kama karoti iliyokatwa vipande vidogo vidogo, vitunguu na karoti.
Pishi lianze
Washa jiko lako. Hakikisha moto ni wa wastani ili kuepusha kubabua au kuunguza chapati zako
Injika kikaango jikoni na uweke mafuta ya kupikia kijiko kimoja au viwili vya chakula kisha sambaza mafuta hayo yaenee kikaangoni.
Kusambaza mafuta kunasaidia chapati kung’ang;ania kwenye kikaango na kuungua.
Mimina uji kwenye kikaango. Unaweza kutumia kipimo cha kipawa ili kuwa na chapati zitakazoiva vizuri.
Ukimimia uji huo, usambaze kwenye kikaango na kisha subiria dakika moja kabla ya kugeuza.
Hii husaidia kuipa chapati nafasi ya kuiva vizuri na kupata umbo la duara.
Usiweke mchanganyiko mwingi kwa wakati mmoja, kwani kufanya hivyo hufanya chapati kuwa nene, na kusababisha kuchelewa kuiva au kutoiva vizuri kwa sehemu ya kati ya chapati yako.
Subiri kwa sekunde kumi na tano au hadi utakapojiridhisha kuwa mchanganyiko wako umeanza kukauka, kisha geuza upande wa pili.
Weka mafuta kwenye kingo za chapati ili yasambae kuingia kati.
Endelea kugeuza hadi chapati yako itakapopata rangi ya kahawia, na utafanya vivyo hivyo kwa mchanganyiko uliobaki.
Hadi hapo kitafunwa chako kitakuwa tayari.
Umeona ilivyo rahisi!? Kumbe hata wewe unaweza.
Unaweza kujifunza zaidi kupitia kipindi cha Rodgers George ambaye alipika chapati hizo na maini.
Wewe unapendelea kusindikiza chapati za maji na nini?, je ni chai ya rangi, maziwa au sharubati ? tupe maoni yako.