Je, wewe ni mmoja wa wale wanaoepuka kununua viazi mviringo vingi sokoni kwa hofu ya kuharibika haraka?
Kama unakutana na changamoto hii Usijali! Jikopoint tupo kwa ajili yako tukikuletea mbinu zitakazokusaidia kuhifadhi viazi mbatata kwa muda mrefu bila kuharibika.
Mbinu hizi zitakusaidia kuwa na ujasiri wa kununua viazi vingi kwa pamoja ukienda sokoni na kukupunguzia safari za mara kwa mara za kutafuta viungo hivi muhimu katika maandalizi ya aina mbalimbali za msosi.
Katika mwezi huu wa mfungo wa ramadhani na kwaresma mbinu hizi zitakurahishia mapishi na kuokoa muda wa kwenda mara kwa mara sokoni.
Hifadhi viazi katika eneo lenye baridi na giza, kama vile chumbani au sehemu isiyo na mwanga mkali wa jua.
Tovuti ya masuala ya afya ya healthline inabainisha kuwa mwanga au miale ya jua inaweza kusababisha ngozi za viazi kuzalisha klorofili na kupata rangi ya kijani ambayo husababisha uzalishaji mkubwa wa kemikali yenye sumu inayoitwa solanine.
Mbali na kuharibu viazi, kemikali hiyo inaweza kusababisha mlaji kupata kichefu chefu, kuharisha, kutapika na wakati mwingine kuoiteza maisha.
Hivyo ili viazi vyako viwe salama na uvihifadhi kwa muda mrefu hakikisha unaviweka sehemu yenye hewa ya kutosha ili kuzuia unyevunyevu
Epuka kuhifadhi viazi kwenye vyombo vya plastiki au mifuko ya plastiki. Badala yake, tumia mifuko ya karatasi ambayo husaidia kupunguza unyevunyevu na kuwezesha hewa kupita kwa uhuru.
Hii husaidia viazi kukauka vizuri na kuzuia kuharibika mapema.
Mifuko ya plastiki inaweza kushikilia unyevu mwingi na kusababisha viazi kuoza kwa haraka.Pia, mifuko hiyo huchochea kuzaliana kwa fangasi ambao huathiri ubora wa viazi.
Kwa kutumia mifuko ya karatasi, viazi vitadumu kwa muda mrefu na kubaki katika hali bora kwa matumizi.
Kamwe usioshe viazi kabla ya kuvihifadhi, kwani unyevu unaweza kusababisha uharibifu wa haraka.
Ikiwa umelima viazi mwenyewe, ondoa udongo taratibu bila kutumia maji na uhifadhi viazi vikiwa vikavu.
Osha viazi tu pale unapotarajia kuvitumia kupika.
Hakikisha viazi vinahifadhiwa katika sehemu yenye hewa ya kutosha ili kupunguza unyevu unaoweza kuharibu ubora wake.
Ukizingatia hili, utahakikisha viazi vyako vinadumu kwa muda mrefu bila kuoza au kushikana na kuharibika.
Kwa wakulima au wafanyabiashara wa viazi, njia bora ya kuhifadhi viazi kwa muda mrefu ni kutumia ghala la makaa.
Ghala hili linapaswa kuwa na mfumo wa kupoza kwa njia ya mkaa uliojaa unyevunyevu wa kudhibiti joto.
Kuta za ghala zinapaswa kuwa na waya wa vyavu uliojazwa mkaa, ambao utahifadhi unyevunyevu unaosaidia kuweka hali ya baridi ndani ya ghala.
Pia, hakikisha magunia hayagusani na kuta za ghala ili kuzuia kuharibika kwa viazi, mbinu hii inaweza kukusaidia kuhifadhi viazi kwa miezi tatu hadi minne
Viazi vinapaswa kuhifadhiwa mbali na mboga au matunda yanayotoa gesi ya ethilini kwa wingi, kama vile tufaa, parachichi, peasi, na aprikoti.
Gesi hii inaweza kusababisha viazi kuanza kutoa mizizi na kubadilika ladha, hata wakati mwingine kuwa sumu.
Hakikisha unavihifadhi katika sehemu tofauti na matunda hayo ili kuepuka athari mbaya za gesi inayotolewa.
Viazi vikiwa katika joto la baridi kali, wanga wake hugeuka kuwa sukari, na kufanya viazi kuwa na ladha tamu isiyofaa na kubadilisha rangi yake wakati wa kupikwa.
Hii inaweza kuathiri ladha na mwonekano wa viazi unapovipika.
Epuka kuhifadhi viazi kwenye friji au freezer isipokuwa kama vimekatwa au kupikwa tayari.
Endapo unaishi katika eneo lenye joto kali, jaribu kutafuta sehemu yenye ubaridi wa wastani badala ya kuviweka kwenye friji.
Epuka kuhifadhi viazi na vitunguu
Ingawa viazi na vitunguu vinahitaji mazingira sawa ya kuhifadhi, haviwezi kuwekwa pamoja.
Vitunguu hutoa gesi inayoweza kuchochea viazi kuota haraka, hivyo ni vyema kuvihifadhi sehemu tofauti.
Njia bora ya kuhakikisha viazi vinadumu kwa muda mrefu ni kuvihifadhi kwenye kikapu au sehemu tofauti na vitunguu.
Kwa kufanya hivi, utaepuka kuoza au kuchipua kwa haraka kwa viazi vyako..
Ikiwa unashangaa iwapo viazi vyako vimeharibika, angalia kama viazi vina ukungu, madoa meusi, au sehemu laini, kuwa na sura ya kunyauka au kumomonyoka.
Aidha, kubadilika rangi kuwa kijani ni ishara ya kuwepo kwa solanine, ambayo inaweza kuwa hatari kwa afya. Hivyo hakikisha viazi vilivyo na rangi hii havitumiki ili kuepuka madhara ya kiafya.
Kwa sasa unajua mbinu bora za kuhifadhi viazi! Je, una mbinu nyingine za kuhakikisha viazi vinadumu kwa muda mrefu?