Kwanini staili za uandaaji viungo zinatofautiana

Na Maria Acley
3 Feb 2022
Ukataji wa viungo unatakiwa kuendana na pishi unalopika. Mfano, viungo vyembamba vinapendeza kwenye kachumbari.
article
  • Kila namna ya ukataji inachangia katika uivaji wa viungo hivyo.
  • Maumbo makubwa ni kwa ajili ya vyakula ambavyo unapenda viungo vionekane.
  • Kukata viungo vidogo ni kama unataka vipotelee kwenye pishi lako.

Kila siku katika jiko langu nimekua nikikwambia mara kata karoti hivi, mara hoho vile, mara ooh utakata utakavyopenda. 

Leo nataka nikuoneshe na kukuelekeza namna mbali mbali za kukata viuongo vyako jikoni na kwanini ufanye hivyo.

Tutajifunza namna ya kukata karoti, hoho na kitunguu.

Unaweza kujiulza kwani kuna umuhimu gani au kwanini nikate hivi na sio vile, relax chukua kiti na kinywaji majibu yote utapata hapa.

Maandalizi ya karoti

Kuna namna nyingi sana za kuandaa karoti kutokana na kwamba inatumika kwenye mapishi kedekede. 

Leo tutajifunza namna tatu ambazo unaweza kuandaa karoti na ukatumia kwenye mapishi yako mbali mbali.

Karoti za duara

Uandaaji wa karoti kwa umbo hili unategemeana sana na matumizi. Ninaposema matumizi namaanisha unaitumia kwenye chakula gani au kwenye mboga gani. 

Mara nyingi kama utaandaa karoti zako kwa namna hii basi ni vyema ikawa kwa ajili ya matumizi ya mapishi kama ya wali wa maua, pilau, supu na dagaa.

Mbali na muonekano mzuri katika chakula ukataji huu huweka wepesi wa kuiva na karoti kubaki katika umbo lake 

Kila aina ya ukataji unatakiwa kuendana na pishi lako. Picha| Favourite Family Recipes.

Karoti za urefu

Kuandaa karoti kwa urefu kuna kuna aina mbali mbali ikiwemo nyembamba na nene pia.

Ukubwa au upana wa karoti yako unayoiandaa kwa urefu unategemeana na unahitaji kuitumia kwenye chakula gani. 

Karoti nyembamba mara nyingi inatumika kwenye kachumbari kutokana na kwamba haimpi shida mtumiaji na ni rahisi kutafunika.

Zenye upana zaidi hutumika kwenye makange, mboga nyingi pia waweza kutumika karoti zenye umbo hili.

Karoti ya kusaga

Namna hii ya uandaaji wa karoti ndio namna inayotambulika kwa wengi na wengi hutumia kwenye kila pishi. 

Hii ni kwasababu ni nyepesi sana lakini pia ni rahisi sana kuiva na kuacha ladha yake kwenye pishi lako.

Njia hii ni nzuri kwa ambao hawapendi kutafuna karoti wakati wa kula kwani kiungo hicho huiva na kupotelea kwenye mchuzi.

Maandalizi ya hoho

Baada ya kuona namna tatu za  kuandaa karoti na kila aina inatumika kwenye pishi gani, sasa tuende kwenye upande wa hoho.

Katika uandaaji wa hoho nako kuna aina mbali mbali za kuziandaa na kuna maumbo mbali mbali ambayo hoho hukatwa.

Uzuri wa kila aina ya uandaaji wa hoho hauna kikomo cha matumizi isipokuwa tu zile zinakatwa kwa ajili ya makange, ambazo hukatwa kwa urefu lakini tofauti na hapo unaweza kukata ama kuandaa hoho zako kwa namna yoyote unayoipenda na ukatumia katika chakula chochote.

Hizi ni baadhi ya namna ambazo unaweza kuandaa hoho zako.

Kumbuka kuweka hoho mwishoni mwa pishi lako ili kubakiza virutubisho. Picha| Savory Nothings.

Hata hivyo, kwa mtu ambaye hapendi kutafuna hoho kubwa kwenye mboga zake, anaweza kuikata nyembamba hasa kwenye kachumbari.

Maandalizi ya vitunguu.

Maandalizi ya vitunguu kwa matumizi ya mapishi nayo hayaendi mbali sana na hoho. Katika uandaaji wa vitunguu waweza kukata kwa style yoyote ile iwe vikubwa, vidogo au hata vya kati. 

Ila kitu kimoja tu cha muhimu katika kukata vitunguu kwa maumbo madogo madogo ni uivaji wake, vitunguu vilivyokatwa kwa maumbo madogo ni rahisi sana kuiva na kutoonekana kwenye mboga ukilinganisha na maumbo mengine.

Hizi ni namna mbali mbali za uandaaji wa vitunguu.

Baada ya kusoma maelekezo haya natumaini katika maandalizi ya viungo sasa utakua unaandaa kila kiungo kutokana na nini unapika lakini pia kipi unapenda.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa