Huenda unadhani unahitaji sufuria maalumu ili upike mboga na chakula chako kwa kutumia mvuke.
Hapana, wakati mwingine vyombo vya nyumbani vinatosha kabisa kukuwezesha upike mboga zako za majani kwa njia ya mvuke.
Mahitaji
1: Sufuria kubwa.
2: Bakuli lenye kitako kipana.
3: Chujio la bati lisilo na mshikio au chuujio la nazi.
4: Mfuniko unaotosha vizuri kwenye sufuria.
Kazi ianze
Weka maji kwenye sufuria na kisha bandika sufuria jikoni. Kalisha bakuli ndani ya maji hayo na ni vyema bakuli likawa katikati ya sufuria.
Washa moto ili kuruhusu maji yachemke na kisha anza kuandaa mboga yako.
Kwa mboga za majani ambazo zinahitaji chumvi unaweza kutumia njia ya sufuria ndani ya sufuria. Yaani badala ya chujio, tumia sufuria.
Maji yakichemka, weka mboga unayotaka kupika kwenye chujio na kisha ukalishe chujio hilo kwenye bakuli ndani ya sufuria.
Funika sufuria na unaweza kuweka kitu kizito juu ya mfuniko ili kutokuruhusu kabisa mvuke utoke.
Kwa njia hii mboga za majani zinahitaji dakika 10 hadi dakika 15. Baada ya hapo funua sufuria na utoe mboga zako. Unaweza kuwa unageuza mara moja moja wakati ukisubiri.
Utake nini tena? JikoPoint ndiyo mambo yote.