Njia sahihi za kusafisha jiko la umeme

Na Mwandishi Wetu
10 Dec 2021
Mbali na kuwa na vifaa maalumu vya kusafishia, ni muhimu kusafisha jiko la umeme kila baada ya matumizi.
article
  • Unatakiwa kuwa na nyenzo maalumu za usafi.
  • Pata ushauri wa wataalam kabla ya kusafisha.
  • Safisha kila baada ya kulitumia ili libaki safi.

Dar es Salaam. Jiko la umeme la kupikia ni miongoni mwa nishati safi na salama zinazopendekezwa kwa sababu zinaokoa mazingira na kulinda afya ya mtumiaji.

Hata hivyo, likitumika kwa muda mrefu huchafuka na mtumiaji asipokuwa makini kulisafisha mara kwa mara linaweza kuchakaa kwa haraka.

Endapo jiko lako limepoteza muonekano wake wa awali kwa kuwa na uchafu sugu, habari njema ni kuwa zipo njia unazoweza kutumia kusafisha jiko lako.

Endelea kusoma makala haya kujifunza mbinu za kusafisha uchafu sugu kwenye sahani za jiko na dondoo za kukusaidia usifubaze jiko lako.

Unawezaje kuepuka uchafu sugu kwenye jiko lako la umeme?

Ukweli ni kwamba uchafu kwenye jiko hauwezi kuepukika kwani katika kupika kuna uji kumwagikia jikoni, mchuzi wa mboga kudondoka wakati wa kupakua na hata mafuta kurukia jikoni wakati wa kukaanga vitu.

Jiko likiwa safi muda wote ni faida kwani litadumu muda mrefu. Picha| Spoon University.

Licha ya kuwa uchafu hauepukiki, unaweza kuepusha jiko lako kuchakaa mapema kwa kutumia mbinu hizi:

1: Safisha jiko lako kila baada ya matumizi

Ni rahisi kupotezea uchafu kidogo unaobaki kwenye jiko baada ya kupika. Mchuzi, mafuta na vitu vingine lakini huenda unapoganda ikakuwa vigumu kuusafisha ukikaa muda mrefu.

Na endapo hautausafisha kwa wakati, huenda uchafu huo ukawa sugu kwenye jiko lako. Jitahidi kila ukipika liache jiko lako katika hali ya usafi.

Tovuti ya Oven Clean inashauri kuwa, kusafisha jiko kila baada ya matumizi kutalifanya jiko lako liendelee kung’aa siku zote.

“Kusafisha uchafu mdogo kila baada ya kupika kutaondoa ulazima wa usafi mzito,” imeandika Oven Clean. 

2: Tumia vifaa maalumu vya kusafisha majiko

Bila shaka unatumia sabuni na kitambaa lakini je ni vya kusafishia majiko? Kila sabuni ina viungo vyake ambavyo vinafanya kazi zaidi kwenye malighafi fulani.

Mathalan, kuna sabuni za kioo, aluminium, chuma na plastiki. Kwa majiko ya umeme nayo yametengenezwa kwa malighafi yake ambayo pia unahitaji sabuni yake.

Inashauriwa kutumia sabuni sahihi kusafishia sehemu za jiko lako ili kupata matokeo mazuri. Wapo ambao hutumia waya wa chuma cha pua (steel wire) maalumu kwa kusugulia sufuria na kusishia kuchubua sehemu na rangi za majiko.

Chukua muda, ongea na mtaalamu na fanya maamuzi sahihi unaponunua vifaa vya usafi wa jiko lako.

Kuwa na siku malumu ya usafi kutakusaidia kufikia sehemu ambazo huwa unazipita. Picha| Good Housekeeping.

3: Andaa siku maalumu ya usafi

Usafi wa kila siku haufiki kila sehemu ya jiko. Hauwezi kuniambia kuwa huwa unasogeza jiko lako kila siku na kusafisha uvungu wake, kufuta sehemu ya kuokea hata kama haijatumika, kufuta sehemu ya nyuma na sehemu zingine.

Kwa usafi wa kila siku, bila shaka huwa unaishia sehemu ya juu tu ya jiko.

Tovuti ya kampuni ya usafi ya  nchini Uingereza ya brightnshinyovencleaners inaeleza kuwa, kushindwa kufanya usafi mzuri wa jiko lako kunaweza kusababisha mrundikano wa uchafu katika sehemu ambazo hazifikiwi mara kwa mara.

Hivyo kuwa na siku maalumu kwa ajili ya usafi wa jiko lako kutakuepusha na uchafu sugu hasa wa sehemu ambazo hazionekani kwa urahisi. 

Mbali na hilo, itaepusha madhara kwenye jiko lako ikiwemo kuvutia wadudu kama mende na panya.

Ungelipenda kujua nini zaidi kuhusu majiko ya umeme? Tuandikie kupitia kurasa za mitandao ya kijamii au WhatsApp kupitia +255 677 088 088.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa