Unavyoweza kuchemsha maji ya kunywa pasipo kutumia mkaa

Na Mwandishi Wetu
11 Mar 2022
Kuchemsha maji siyo lazima kwenye mkaa tu. Unaweza kutumia nishati kama gesi, umeme na teknolojia zingine.
article
  • Ni kwa kutumia majagi ya umeme.
  • Gesi, jiko la umeme siyo ghali kama unavyodhani.
  • Zipo mashine za kuchuja maji zinazoweza kukufaa.

Kwa baadhi ya familia, ikifika siku ya kuchemsha maji ya kunywa, basi mkaa utanunuliwa ili utumike kwa ajili ya kuchemshia maji hayo.

Wengi huona kuchemsha maji ya kunywa kwenye jiko la umeme au la gesi ni gharama kubwa ikilinganishwa na kununua mkaa wa Sh2000, jambo ambalo siyo kweli.

Kwa kawaida, kuchemsha maji yakatokota na kufaa kunywa huanza na maandalizi ya muda mrefu, kuanzia kuutafuta mkaa wenyewe, kuuwasha na kungojea hadi ushike moto na pia ulazima wa kuongeza mkaa kwenye jiko ili uchemshe maji mengine. Ni usumbufu.

Hizi ni njia rahisi zaidi za kupata maji ya kunywa bila uhitaji wa mkaa

Yapo majagi ya kuchemsha maji kwa umeme ya lita tan na zaidi. Picha| Jiji.Ug.

Tumia jagi za umeme za kuchemshia maji

Hii itawafaa zaidi mabachela na wale wenye familia ndogo, tuseme za watu watatu au wanne.

Kama una miliki jagi la kuchemshia maji la lita mbili, inamaanisha utachemsha maji ya lita 1.7 kwa wakati mmoja na utachukua takriban dakika 6 kukamilisha.

Kujaza ndoo ya lita 10, utachemsha walau mara sita tu na hivyo kuchukua dakika 40 kukamilisha zoezi la kuchemsha maji bila haja ya kukoleza jiko wala kuwa na safari ya kutafuta mkaa. Pia kumbuka, ukitumia mkaa utatumia muda mwingi zaidi.

Kuna majagi ya umeme ya kuchemshia maji ya hadi lita tano hivyo ni wewe na uchaguzi wako tu.

Majagi haya yanaweza kutumika kwa hadi miezi sita. Picha| Prozis

Nunua mashine za kuchuja maji

Baadhi ya familia zimeshasahau kabisha adha ya kununua maji wala kuchemsha baada ya kununua mashine zinazotakasa maji. 

Mashine hizi ziimetengenezwa kwa ujazo tofauti kuanzia jagi la lita tatu hadi lita 10. Kwa lugha ya kitaalamu, zinaitwa water filter au purifier. 

Kwa mujibu wa tovuti ya bbc good food majagi haya ya kuchuja maji yanaweza kudumu kwa hadi miezi sita kabla ya kubadilisha. 

Kuchemsha maji kwenye gesi unahitaji nusu saa kuwa na maji lita kumi. Picha| Google Images.

Gesi, umeme siyo ghali kama unavyodhani

Baadhi ya watu wanadhani kuchemsha maji kwenye gesi au kwenye jiko la umeme inatumia muda mrefu sana na hivyo kutumia nishati nyingi. Siyo ukweli.

Kuchemsha maji ya lita moja kwenye jiko la gesi, unahitaji walau dakika sita hadi nane. Kitu ambacho ni sawa au chini ya kurosti nyama.

Hivyo ni kusema, ukitenga kama saa moja, una uwezo wa kuchemsha maji mengi tu ya kutumia kwa muda mrefu.

Haya sasa, natumaini utapunguza matumizi ya mkaa au gharama za kununua maji ya dukani kwa kuzingatia dondoo hizi.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa