Baadhi ya watu hupendelea kusema Sikukuu hainogi bila uwepo wa nyama mezani.
Kauli hii inaweza kuungwa mkono na mamia au maelfu ya walaji wa aina mbalimbali za nyama ikiwemo nyama ya ngombe, ya kuku na nyingine nyingi.
Licha ya umuhimu wa nyama katika kunogesha sikuukuu huenda baadhi ya watu wakashindwa kumudu kutokana na kupaa kwa gharama zake.
Katika baadhi ya masoko jijini Arusha kilo ya nyama ya ng’ombe huuzwa kwa Sh 12,000 na zaidi wakati kuku wa kisasa akiuzwa kuanzia Sh 9,000 hadi Sh10,000.
Kwa wale wapenzi wa kuku wa kienyeji kuelekea msimu huu wa sikukuu unaweza kupata kwa bei ya Sh23,000 hadi Sh25,000.
Akizungumza na jikopoint mmoja wa wauzaji wa nyama ya ng’ombe katika soko la Morombo jijini Arusha aliyejitambulisha kwa jina la Fadhili amesema kitoweo hicho kimeanza kupanda bei kuanzia wiki tatu zilizopita.
“Wiki tatu zilizopita nyama tulikuwa tunauza kilo 10,000 Hadi 9,000 ila sasa hivi kama unavyoona…sababu ya kupanda kwa bei ni kuongezeka kwa gharama za uagizaji nasisi wenyewe tunapochukulia bei ipo juu,” amesema Fadhili.
Jikopoint imekuandalia mbinu nne zitakazokusaidia kupunguza matumizi ya kupanda kwa gharama ya nyama nchini na kunogesha sikukuu za mwisho wa mwaka katika familia yako.
Nunua nyama mapema
Kwa mujibu wa utafiti mdogo uliofanywa na Jikopoint gharama.za chakula na vinywaji huwa na kawaida ya kupaaa inapokaribia msimu wa sikukuu hivyo njia bora ya kudhibiti hali hiyo inaweza kuwa kununua mahitaji yako ikiwemo nyama mapema.
“Kwa mwenendo huu wa bei ya nyama unavyoonekana mpaka kufikia sikukuu bei itakuwa haishikiki,” amesema muuzaji mwingine wa nyama alijitambulisha kwa jina la Moses Kirwai.
Ikiwa unafahamu matumizi halisi ya nyama katika familia yako unaweza kununua mapema hata wiki moja kabla Kisha ukahifadhi katika jokofu ukisubiri sikukuu ifike.
Tembelea kwenye minada au kwa nunua kwa wafugaji
Ikiwa una familia kubwa manunuzi ya nyama katika mabucha ya kawaida yanaweza kutoboa mifuko yako zaidi hivyo unaweza kutembelea minada ya mifugo ambapo huuzwa kwa bei rahisi kidogo itakayorahisha upatikaji wa kitoweo hicho kwa gharama nafuu.
Mathalani kuku wa kienyeji anayeuzwa Sh 28,000 unaweza kupata kwa bei ya chini hadi Sh 25,000 pia ukapata nafasi ya kuchagua ubora unaouhitaji.
Unaweza kutumia mbinu hii pia kujipatia aina nyingine za mifugo yenye ukubwa na gharama unazoweza kumudu kama vile mbuzi, bata na kondoo.
Nenda machinjioni
Kwa wakazi wanaoishi maeneo yaliyopo jirani na machinjio hii inaweza kuwa fursa ya kupunguza gharama za kitoweo msimu huu wa sikukuu kwa sababu maeneo hayo huuza nyama kwa bei rahisi kulinganisha na mabucha ya mtaani au sokoni.
Punguza Vyakula vinavyotumia nyama
Unaweza kubuni mapishi mbadala yanayotumia aina nyingine ya vitoweo ikwemo samaki na nafaka kama njegere ili kupunguza matumizi ya nyama msimu wa sikukuu.
Unaweza kuandaa mapishi kama pilau la prawns, wali wa maua, wali wa manjano, ambayo yote yanapatikana katika tovuti yetu jikopoint.co.tz.