Unavyoweza kutengeneza ‘milkshake’ ya embe

Na Lucy Samson
13 Jan 2023
Juisi hii ya embe na maziwa inampatia mtu faida nyingi mwilini ikiwemo madini ya chuma, protini na vitamin C.
article
  • Kinywaji hiki ni chanzo kizuri cha vitamini C, protini na madini chuma.
  • Kinafaa kutumiwa na watu wa rika zote.
  • IIi kuitengeneza utahitaji blenda yenye uwezo wa kusaga vitu vigumu.

Juisi za matunda ni moja ya kinywaji kizuri kinachoweza kutumiwa wakati wote na watu wa rika zote isipokuwa wale wenye mzio na changamoto nyingine za kiafya.

Uzuri wa juisi hizi unaweza kutengeneza nyumbani kwa gharama ndogo ukilinganisha na juisi za viwandani ama vinywaji vingine.

Kabla ya msimu wa maembe haujaisha tutengeneze milkshake ya embe (juisi yenye mchanganyiko wa maziwa na embe) yenye faida nyingi mwilini ikiwemo madini ya chuma, protini na vitamin C.

Fuatana nami kujifunza namna ya kuandaa kinywaji hiki pendwa chenye ladha ya kipekee.

Maandalizi

Osha embe, (maembe) menya na ukatekate vipande vidogo vidogo vitakavyoweza kusagika kwa haraka.

Andaa blenda, weka matunda yako, kikombe kimoja cha maziwa, vipande vya barafu na aina yoyote ya ladha unayopendelea kisha usage mpaka matunda yalainike.

Moja kati ya sifa ya milkshake nzuri ni kiwango cha ulaini (softness) unachoweza kukipata ikiwa utasaga kwa muda mrefu.

Hakikisha blenda unayotumia iwe yenye uwezo wa kusaga vitu vigumu (heavy duty blender) ili kurahisisha mchakato wa matunda kusagika.

Ikiwa unatumia blenda ya kawaida utalazimika kurudia kusaga mara mbili au zaidi ili maembe yasagike vizuri kwa sababu aina hii  ya juisi haichujwi.

Ukishamaliza kusaga unaweza kuweka juisi yako kwenye friji ili ipate baridi zaidi au kuweka kwenye glasi tayari kwa kunywa.

Haina haja ya kuongeza sukari. Embe lina sukari ya kutosha kukuwezesha kufurahia kinywaji hicho.

Unaweza kuongeza urembo wa vipande kadhaa vya embe, au jani la mnanaa (mint) juu ya glasi ili kuongeza muonekano mzuri.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa