Vinywaji vya kuepuka wakati wa ujauzito

Na Lucy Samson
15 Jul 2022
Vinywaji vyenye vilevi, vya kuongeza nguvu, vyenye kafeine na maziwa yasiyo salama.
article
  • Unywaji wa vilevi na vinywaji vyenye kafeini.
  • Badala yake mama mjamzito anywe maji mengi na juisi za matunda.

Zipo baadhi ya dhahania kuwa mwanamke akiwa mjamzito haruhusiwi kunywa  hiki au kile, huku sababu kubwa ikiwa ni mwiko kunywa vinywaji  hivyo.

Wote wenye mtazamo huo wana sababu mbalimbali ambazo hutegemea kiwango cha elimu, mila na desturi. 

Sasa tuachane na maoni ya wazee na wanajamii, Dk Lucy Ogutu, kutoka Kaloleni Dispensary Arusha, anasema mjamzito anapaswa kutumia makundi yote ya chakula kwa kiasi ili kupata virutubisho vyote. 

“Mjamzito anabidi atumie anatakiwa atumie makundi yote ya chakula kama wanga, protini na vitamini kwa kiasi, vyakula au vinywaji asivyotakiwa kutumia ni vile vinavyomdhuru yeye na mtoto aliye tumboni,” anasema Dk Ogutu.

Kwa mujibu wa jarida la healthline, kipindi cha ujauzito ni kipindi ambacho mjamzito anatakiwa azingatie aina ya chakula au kinywaji anachokunywa, ili kumlinda mtoto aliye tumboni.

Makala hii inaangazia aina ya vinywaji hatarishi visivyoshauriwa kutumiwa  na mama mjamzito kipindi chote cha  ujauzito wake:

Kahawa

Jarida la healthline linaeleza kuwa kahawa ni moja ya kinywaji chenye kiwango kikubwa cha kafeini ambayo ikitumiwa kwa wingi, huongeza shinikizo la damu na mapigo ya moyo, ambayo yote hayapendekezwi wakati wa ujauzito.

“Mjamzito hashauriwi kutumia zaidi ya miligramu 200 ya kahawa,” limeeleza jarida hilo.

Miligramu 200 ni sawa na nusu kijiko cha chakula au vijiko 2 vidogo vya chai. Ikishindikana kabisa kuacha kutumia kahawa basi atumie chini ya kiwango hicho.

Vilevi havishauriwi kutumiwa na akina mama wajawazito kwa sababu vinaweza kusababisha madhara mwilini. Picha| Mtandao.

Vinywaji vya kuongeza nguvu

Vinywaji vya kuongeza nguvu hutumiwa sana pale mtu anapochoka au kuwa na usingizi wakati akihitajika kufanya majukumu mengine.

Vinywaji hivi huwa vimebeba kaffeini ambayo haihitajiki kwa kipindi cha ujauzito. 

Kafeine iliyopo kwenye vinywaji vya kuongeza nguvu, huongeza mzunguko wa  mkojo kwenye kibofu, hali inayopelekea kupata haja ndogo mara kwa mara na kusababisha kupungua kwa viwango vya maji mwilini.

Kafeini inaweza kuvuka plasenta hadi kufikia mtoto aliye tumboni. 

Vilevi

Vilevi vya  aina zote havishauriwi kutumiwa kipindi cha ujauzito. Kwa mujibu wa mtaalamu wa chakula na lishe Kivyera Banduka, anasema mama mjamzito akitumia  vilevi  anaweza kumsababishia madhara mtoto aliye tumboni. 

“Unywaji wa vilevi au pombe wakati wa ujauzito huongeza hatari ya kuharibika kwa mimba na kuzaa mtoto aliyekufa, au kuathiri ukuaji wake,” amesema Banduka.

Jarida la healthline linafafanua kwamba hakuna   chanzo cha  kuaminika ambacho kimethibitisha kiasi cha kilevi cha kutumia  wakati wa ujauzito, hivyo inashauriwa kuepuka kabisa matumizi ya pombe.

Maziwa yasiyo salama (unpasteurized milk)

Kuna baadhi ya mazingira yanaweza kumlazimisha mama mjamzito anywe maziwa yasiyoiva au yasiyo salama (unpasteurized milk). Hali hiyo inayoweza kuongeza bakteria ambao wanaweza kumdhuru mama mjamzito na mtoto aliye tumboni.

“Wanawake wajawazito wana hatari kubwa ya kuugua kutokana na bakteria listeria, ambayo mara nyingi hupatikana katika maziwa mabichi na inaweza kusababisha kuharibika kwa mimba, au ugonjwa, au kifo cha mtoto mchanga.” amesema Banduka.

Matunda, mboga za majani ni miongoni mwa vyakula anavyoshauriwa mama mjamzito kutumia ili kumpatia virutubisho mwili. Picha| Happy Family Organics.

Vinywaji vipi watumie?

Wataalamu wa afya wameshauri baadhi ya vinywaji ambavyo mama mjamzito anapaswa kutumia kwa ajili ya maendeleo mazuri ya mtoto aliye tumboni na kuimarisha afya yake kwa ujumla.

Maji safi na salama

Maji ni kinywaji muhimu kwa binadamu yoyote kama ambavyo sisi watu wazima tunahitaji maji hivyo ni sawa na mtoto aliye tumboni. Hivyo mjamzito anashauriwa kunywa maji mengi.

“Wanawake wajawazito wanahitaji maji zaidi kuliko mtu wa kawaida ili kusaidia mzunguko wa kiumbe kilicho tumboni  na  uzalishaji wa damu ya ziada,” limeeleza jarida la Healthline.

Juisi za matunda (Fresh juice)

Kipindi cha ujauzito ni kipindi ambacho mamaanatakiwa kuongeza vitamini na virutubishi vingine ambavyo baadhi hupatikana kwenye juisi za matunda.

Matunda hayo yanapaswa kuoshwa vizuri na kuandaliwa katika hali ya usafi ili kumpa mama mjamzito virutubisho vinavyohitajika.

Dk Joseph Ponda kutoka kutoka Kituo Cha Afya Tabata jijini Dar es Salaam anasema vinywaji na vyakula anavyokula mjamzito ni lazima viandaliwe katika usafi ili kuepusha bakteria wanaoweza kuleta magonjwa.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa