Tumia vyakula hivi ikiwa unapata maumivu makali wakati wa hedhi 

Na Esau Ng'umbi
29 Jun 2022
Vyakula hivyo ni pamoja na mtindi lishe, karanga, nyama, mayai na tikiti maji.
article
  • Vinatajwa kupunguza maumivu ya hedhi kwa kiasi kikubwa. 
  • Utendaji kazi wake unafanana na dawa za viwandani.

Dar es salaam. Zipo nadharia mbalimbali kuhusu hedhi kwa wanawake. Wakati mwingine huwa ni vigumu kuelezea namna gani mtu hujisikia akiwa katika kipindi cha hedhi. 

Baadhi ya wanawake hupata hedhi bila maumivu yoyote na wapo ambao hushindwa hata kuinuka kitandani kutokana na maumivu makali ambayo muda mwingine huambatana na homa. 

Kwa mujibu wa Mtandao wa Linda Afya maumivu hayo hutokana na kutanuka na kusinyaa kwa misuli ya mfuko wa mimba, jambo ambalo huratibiwa na homoni ya “prostaglandins” ambapo wakati wa hedhi misuli husinyaa zaidi na kupelekea hewa ya oksijeni kukosekana kwenye mfuko huo. 

Taasisi ya Flo Health ya nchini Belarus inayojihusisha na utoaji wa elimu ya uzazi kwa wanawake wanashuku kuwa huenda maumivu makali wakati wa hedhi husababishwa na ulaji usiofaa, hivyo wamependekeza baadhi ya vyakula ambavyo husaidia kupunguza maumivu wakati wa hedhi.

Mayai

Mayai yana utajiri mkubwa wa madini chuma, mafuta, vitamini B pamoja na protini ambavyo kwa pamoja husaidia kupunguza maumivu wakati wa mwili unapopitia mabadiliko ya kihomoni.  Hata hivyo, haishauriwi kula mayai ya kuchemsha kwa wingi kwani yanaweza kusababisha gesi au kiungulia.

Tikiti maji

Tunda hili lina sukari ya asilia ambayo inaweza kukusaidia kutotumia vitu vyenye sukari zaidi pamoja na kufanya mwili wako kusalia na maji mengi. Vitamini B6 iliyopo katika tunda hilo  inaweza kupunguza kuwashwa, kutokwa na damu na wasiwasi unaohusishwa na maumivu ya hedhi.

Karanga

Kwa mujibu wa Flo Health, karanga zina asidi nyingi za mafuta ya omega ambayo ni chanzo kikubwa cha protini hivyo inashauriwa karanga zitumiwe kwa wingi wakati wa hedhi.

Tangawizi

Utafiti uliofanywa na Dk Tracy Lookwood mwaka 2009 ambao umechapishwa katika  Kitabu cha Suluhu ya Vyakula wakati wa Hedhi, naonesha wanawake 150 waliotumia gramu moja ya unga wa tangawizi kwa siku tatu za kwanza za kipindi cha hedhi, kiungo hicho kilipunguza maumivu kwa ufanisi kama vile dawa za kutuliza maumivu aina ya  “buprofen.”

Mtindi lishe 

Mtindi lishe (probiotic Yoghurt ) una kalsiamu nyingi ambayo husaidia kupunguza maumivu ya hedhi kwa sababu huwa na bakteria rafiki ambao husaidia mmeng’enyo wa chakula na hupunguza uvimbe.

Utafiti wa Dk Lookwood umeonesha lishe inayopatikana kwenye mtindi husaidia kupunguza maumivu wakati hedhi kwa asilimia 40.

Nyama 

Ni kawaida sana kwa wanawake kukosa madini ya chuma wakati huu wa hedhi na dalili kuu ni kuhisi kuishiwa nguvu hivyo nyama nyekundu ni miongoni mwa vyanzo tajiri vya madini ya chuma, hivyo inashauriwa kula nyama kwa wingi kwani ni muhimu kwa wanawake hasa wanaokabiliwa na hedhi nzito.

Kama hupendelei nyama nyekundu, unaweza kula mchicha kwa wingi, dengu au maharage.

Nyama husaidia kuongeza protini mwilini na kumpa mwanamke nguvu wakati wa hedhi. Picha| Mtandao.

Dk Ken Nyabugi kutoka kituo cha tiba mbadala cha Afya Kwetu kilichopo Ilala Sokoni  jijini Dar es Salaam, amesema matatizo mbalimbali yanayohusiana na hedhi, yanaweza kudhibitiwa na hatimaye kutokomezwa kabisa kwa kutibu mfumo mzima wa mwili.

Hii hufanyika kwa kuondoa sumu iliyojilimbikiza katika mwili wa mgonjwa kwa kipindi cha muda mrefu.

Dk Nyabugi amesema kuwa mfumo mzima wa mwili unapokuwa umezingirwa na sumu (toxins), ndiyo huwa chanzo cha matatizo mbalimbali, yakiwemo hayo yanayojitokeza kwa wanawake wakati wa hedhi na dawa pekee katika hili ni kwanza, kuondoa sumu hizo mwilini kwa njia ya lishe.

“Ili kuondoa sumu hizo mwilini, mgonjwa anatakiwa kuanza mpango maalum wa kula matunda na mbogamboga pekee,” amesema Dk Nyabugi.

Katika siku hizo, anachokuwa anakula ni matunda, juisi za matunda kama machungwa, mananasi, zabibu, tufaa, papai bichi, karoti, parachichi, nyanya, mboga mbalimbali pamoja na maji.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa