Jinsi ya kutengeneza juisi ya “apple” 

Na Rodgers George
7 Mar 2022
Kutengeneza juisi hii utahitaji Sh3,000 kwa ajili ya kununua matunda.
article
  • Unahitaji mashine ya Juicer au blenda inayoweza kusaga vitu bila maji.
  • Utaichuja kama ulitumia blenda lakini kwa juicer hamna haja ya kuchuja.
  • Juisi hii ni nzuri kwa watu wenye changamoto za afya ikiwemo  kisukari.

Huenda unafahamu kutengeneza juisi nyingi lakini juisi ya tufaha au wazungu huliita “apple” ni kati ya juisi ambazo huzikuti sehemu nyingi wanaouza vinywaji.

Leo nitakufundisha ujanja huu ili usibaki ukizunguka kwenye vinywaji vile vile kila siku.

Mahitaji 

1. Juicer/ blenda

2. Tufaha tatu

3. Chujio 

4. Kontena

Kama unatumia “juicer”, kata matufaha yako kwa umbo la robo. Picha| Juice Buff.

Jinsi ya kutengeneza kinywaji

Osha matunda yako vizuri na unaweza kutumia maji ya uvuguvugu endapo hautomenya maganda.

Katakata matunda yako kwa mtindo wa robo kama utatumia juicer (mashine ya kusaga juisi kwa kukuna tunda) na vipande vidogo vidogo kama utatumia blenda.

Kwa juicer, weka kipande kimoja kimoja na uache mashine ikutengenezee juisi yako hadi utakapomaliza vipande vyote.

Kwa blenda, weka vipande vyako vya tufaha kwenye jagi la blenda kisha saga kwa moto mdogo mdogo. Unaweza kutumia batani ya kusaga kwa haraka (pulse) kwa kuanzia.

Kumbuka kuipumzisha blenda yako na siyo kusaga kwa mfululizo.

Baada ya hapo weka kiminika chako kwenye chujio kisha chuja vizuri upate juisi yako.

Unaweza kuongeza mdalasini, sukari au hiriki kama utapenda lakini hadi hapo, kinywaji chako kipo tayari. 

Unaweza kunywa juisi hii sambamba na chakula cha asubuhi, mchana na hata usiku.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa