Jinsi ya kutengeneza juisi ya nazi na nanasi

Na Fatuma Hussein
11 Apr 2025
Unaweza kuweka tangawizi au limao kuongeza ladha zaidi katika juisi.
article
  • Juisi hii inahitaji mahitaji makuu mawili tu ambayo ni nanasi na nazi.
  • Unaweza kuweka tangawizi au limao kuongeza ladha zaidi.

Juisi ya nazi na nanasi ni kinywaji chenye faida nyingi za kiafya, kinachounganisha virutubisho vya matunda mawili yanayopatikana kwa urahisi katika maeneo mbalimbali.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) juisi ya matunda halisi huupatia mwili vitamini na makapimlo yaliyo kwenye matunda halisi husaidia kupunguza uwezekano wa kuugua saratani ya utumbo.

Juisi ya nanasi na nazi ni kinywaji ambacho sio tu kina ladha tamu lakini pia kimesheheni virutubisho mbalimbli ikiwemo vitamini C,  E na vitamini B ambavyo husaidia kuimarisha kinga ya mwili na kusaidia afya ya moyo.

Hatua kwa hatua namna ya kuandaa

Hatua ya kwanza chukua maji safi na salama safisha tangawizi, nanasi na nazi vizuri, kwa nanasi menya maganda kisha ondoa viini vyeusi ili kuhakikisha juisi inakuwa na rangi moja.

Baada ya hapo hatua inayofuata ni kukata kata nanasi katika vipande vidogo vidogo ili wakati wa kusaga iwe rahisi.

Kwa upande wa nazi ipasue na umimine maji yake ndani ya bakuli au kikombe. 

Hatua nyingine ni kukata vipande vidogo vidogo vya nazi ili wakati wa kusaga iwe rahisi hasa kama unatumia blenda ambayo haisagi vitu vigumu.

Baada ya hapo mimina maji ya nazi pamoja na nyama ya nazi/ nazi ndani ya blenda na usage kwa dakika saba mpaka 10 mpaka mchanganyiko ulainike.

Hatua inayofuata ni kuchuja mchanganyiko na chujio safi ili kuondoa machicha. 

Ikiwa una mashine maalumu kwa kutengenezea juisi unaweza kuitumia na ikasadia kuchuja juisi moja kwa moja bila kuhangaika na machujio.

Kwa wenye blenda za kawaida baada ya kupata mchanganyiko wa tui la nazi lililochujwa, weka nanasi, tui la nani na maji ya nazi kwenye blenda kisha saga mchanganyiko huo kwa dakika 10 mpaka 15.

Ukiona huwezi kufuata hatua hiyo saga vipande vya nanasi pamoja na Tangawizi ukipenda sio lazima pembeni kama ulivyofanya awali wakati wa kutengeneza tui la nazi kisha chukua bakuli kubwa na uchuje mchanganyiko huo.

Baada ya kuchuja na kuondoa makapi yote, katika bakuli kubwa changanya juisi ya nanasi na tui la nazi kisha ongeza asali au sukari ukipendelea.

Mpaka hapo juisi itakuwa tayari unaweza kuweka barafu kuipa juisi ubaridi au kuhifadhi katika jokofu kwa matumizi ya baadae.

Kumbuka kinywaji hiki kinafaa zaidi kutumika msimu wa joto kali ili kuupa mwili nguvu.

Bado unasubiri nini? Jifunze, andaa na ufurahie kinywaji hiki cha asili.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa