Juisi ya ‘Smoothie’: Mahitaji, unavyoweza kutengeneza nyumbani

Na Lucy Samson
20 Sept 2022
Smoothies ni juisi ambayo hutengenezwa kwa matunda. Sifa zake kuu huwa ni nzito kuliko juisi za kawaida na husagwa katika blenda maalum.
article
  • Aina hii ya juisi haitumii sukari ya ziada hivyo kupunguza hatari ya kupata kisukari na vitambi
  • unahitaji uwe na blenda ya kusaga vitu vikavu ili kutengeneza juisi hii

“Siku hizi ‘smoothies’ ndiyo habari ya mjini” anasema Agnes Patrick huku akivuta mrija tayari kwa kufurahia juisi yake aliyoitengeneza mwenyewe nyumbani.

Najua nimekuacha njia panda na una shauku ya kujua hii ‘Smoothie’ ndio kinywaji gani? Basi fuatana nami katika makala hii utajifunza hatua kwa hatua jinsi ya kutengeneza kinywaji hiki ukiwa nyumbani kwako.

Smoothies ni aina juisi ambayo hutengenezwa kwa matunda. Utofauti wake na juisi za kawaida ni kwamba aina hii ya juisi huwa nzito sana. Hata aina ya blenda ya kusagia aina hii ya juisi ni tofauti na blenda za kawaida.

“Ni vyema uhakikishe blenda yako ina uwezo wa kusaga vitu vigumu kabla ya kuendelea kutengeneza Smoothie,” anasema Agnes.

Aina hii ya juisi na haina ulazima wa kutumia sukari au  maji mengi ukilinganisha na juisi za kawaida ambazo zinahitaji sukari kwa wingi ili kuongeza ladha na maji mengi yanayorahisha kusaga kwa blenda ya kawaida.

Embe na karakaa yana sukari za asili hiyo hakuna haja ya kuongeza sukari ya ziada wakati wa kutengeneza Smoothie yako.

Kwa mujibu wa Kituo cha Kupambana na Magonjwa (CDC), matumizi ya sukari ya ziada kwenye vinywaji yanaweza kusababisha magonjwa kama kisukari na kuongezeka uzito.  

Hivyo ni vyema ukitumia maji kidogo ili usiongeze sukari ya ziada kwenye Smoothie yako.

Mahitaji ya aina hii ya juisi ni machache tu kutegemeana na idadi ya watumiaji wa kinywaji hicho. Mimi leo nitatumia embe kubwa moja na maparachichi mawili yakayofanya juisi ya watu wawili ikamilike.

Passion fruit and Mango Smoothie - Healthy Thai Recipes
Juisi hii haina haja ya kuchuja,nyuzi nyuzi zilizopo kwenye juisi hii zinasaidia kuboresha mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.Picha|Healthy Thie.

Maandalizi

Hatua ya kwanza ni kununua matunda ambayo ni embe pamoja na karakaa (passion), hakikisha unachagua yaliyoiva vizuri ili kukuwezesha kupata ladha nzuri isiyo na uchachu.

Ukishanunua yaoshe na uyakate kate vizuri vipande vidogo vidogo tayari kwa ajili ya kusaga.

Kama nilivyokudokeza awali, hakikisha blenda yako ina uwezo wa kusaga vitu vikavu kisha iandae kwa ajili ya kusaga embe pamoja na karakaa.

Blenda ikiwa tayari mimina embe na karakaa tayari kwa ajili ya kusaga

Unaweza kuongeza maji robo kikombe kama Smoothie yako imekuwa nzito sana

Ikisagika vizuri mimina kwenye glasi ongeza vipande vya barafu na itakuwa tayari kwa kunywa

Una maswali au una mrejesho baada ya kutengeneza juisi hiyo tucheki Whatsapp kupitia +255 677 088 088 au Twitter, Facebook na Instagram kupitia @JikoPoint au @LucySamsonk.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa