Nishati safi ya kupikia kunusuru maisha ya watu 33,000 kila mwaka Tanzania

Na Lucy Samson
18 Oct 2022
Ni wale wanaovuta sumu inayotokana na matumizi ya kuni na mkaa wakati wa kupikia.
article
  • Ni wale wanaovuta sumu inayotokana na matumizi ya kuni na mkaa wakati wa kupikia.
  • Wadau kujadili suluhu za kutokomeza matumizi ya nishati hatarishi ya kupikia.

Serikali ya Tanzania imesema inaandaa mikakati ya kuondosha matumizi ya nishati hatarishi ya kupikia, hatua itakayosaidia kuokoa maisha ya watu 33,000 kwa mwaka nchini.

Waziri wa Nishati, January Makamba amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam leo (12 Oktoba, 2022) inakadiriwa kuwa watu hao 33,000 wanafariki kutokana na kuvuta sumu zilizopo kwenye moshi unaotoka wakati wa kupika.

“Watanzania walio wengi kwenye upikaji wanameza sumu zinazoingia kwenye mapafu yao…kuna kukosekana kwa haki kwa namna ambavyo tunapika,” amesema Makamba ambaye miezi miwili iliyopita alifanya ziara maeneo mbalimbali Tanzania kuelimisha watu juu ya nishati safi ya kupikia.

Nishati safi ya kupikia inayosisitizwa ni ile isiyo na madhara kwa afya ya mtumiaji wakati wa kupika ikihusisha nishati ya gesi, umeme, mkaa mbadala na nishati ya jua.

Miongoni mwa mikakati watakayofanya ni pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kupunguza ukataji miti kwa ajili ya mkaa na kuni kwa kuwa sehemu kubwa ya kaya nchini wanatumia kupikia. 

Matumizi ya nishati hii yatanusuru maisha ya takribani asilimia 90 ya kaya wanaotumia nishati zisizo salama kuandaa chakula zinazoleta madhara zaidi kwenye afya zao ikiwemo magonjwa ya kifua.

Kuni, mkaa bado zipo Tanzania

“Mpaka sasa asilimia 63.5 ya nishati yote inayotumia majumbani ni kuni, asilimia 26.2 ya nishati inayotumika majumbani ni mkaa,” amesema Waziri Makamba huku akibainisha kuwa tayari Serikali imetenga Sh10 bilioni katika mwaka wa fedha wa 2022/23 kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia. 

Mbali na athari za kiafya ambazo zinachangia uwepo wa zaidi ya theluthi mbili ama asilimia 70 za magonjwa ya upumuaji, matumizi ya nishati zisizo safi yanachangia ongezeko la hewa ya ukaa inayochafua mazingira na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

“Tatizo la namna tunavyopika ni kubwa sana kuliko tunavyolijua, kuliko tunavyolijadili, au tunavyolichukulia hatua…tatizo hili linahusisha mazingira, afya, jinsia na usawa katika jamii,” amesema Makamba.

Licha ya athari hizo bado hali ni mbaya kwenye matumizi ya nishati hiyo nchini ambapo asilimia nane tu au watu wanane kati ya 100 waliopo Tanzania wanatumia nishati safi kwenye matumizi yao ya kila siku kupikia.

Wadau kujadili mustakabali

Katika mkutano huo na wanahabari, Makamba amesema Serikali na wadau wengine watafanya kongamano la nishati safi ya kupikia litakalofanyika kati ya Novemba mosi na 2, 2022 litakalosaidia kuibua suluhu pamoja na kuongeza matumizi ya nishati safi nchini.

“Tunataka tuanze safari ya kupata majawabu ya kudumu ya kuondokana na matumizi ya nishati isiyo safi yenye kuleta athari kwenye mazingira,” amesema Makamba.

Kongamano hilo litahusisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje nchi watakao iwezesha Serikali kupitia Wizara ya Nishati kujua hali sasa iliyopo nchini pamoja na kujadili  njia za kufikia jamii yenye matumizi ya nishati safi. 

Matokeo ya kongamano hilo ni kuweka mifumo ya kisera, kisheria, kikodi mifumo ya kiutawala kupambana na madhara yatokanayo na matumizi ya nishati zisizo safi zinazo athiri afya.

Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa, inayochapisha Nukta Habari na Jiko Point mtandaoni, ni miongoni mwa wadau muhimu wanaohamasisha matumizi ya nishati safi kupitia habari na mafunzo.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa