Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu ameagiza kuundwa kwa kikosi kazi kitakachotoa mwelekeo wa kitaifa juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Kikosi kazi hicho kitakachohusisha sekta binafsi na wadau wa maendeleo kitakuwa na kazi ya kuchambua sera za Serikali na mapendekezo ya wadau mbalimbali kikiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa huku uratibu utafanyika chini ya Wizara ya Nishati.
“Kwenye hili Serikali peke yetu hatuwezi tunapaswa kwenda sambamba na sekta binafsi, nashukuru baadhi yao wameanza kujitokeza,” amesema Rais Samia jana Novemba 1, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mjadala wa kitaifa kuhusu nishati safi ya kupikia.
Lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha inaokoa maisha ya Watanzania wanaofariki kila mwaka kutokana na kuvuta moshi wa kuni.
Inakadiriwa kuwa watu 33,000 nchini Tanzania wanafariki dunia kila mwaka kutokana na kuvuta sumu za moshi unaotoka kwenye kuni na mkaa wakati wa kupika.
Mbali na athari za kiafya ambazo zinachangia uwepo wa zaidi ya theluthi mbili ama asilimia 70 za magonjwa ya upumuaji, matumizi ya nishati zisizo safi yanachangia ongezeko la hewa ya ukaa inayochafua mazingira na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.
Amesema kikosi kazi hicho kitakuja na mpango mkakati ambao utaiongoza Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kutafuta suluhu ya nishati safi na endelevu ya kupikia.
Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, kaya zinazopikia kwa kutumia mitungi ya gesi ni asilimia 5, umeme (asilimia 3) na nishati nyingine safi asilimia 2.2.
“Hii inaonyesha bado kuna kazi ya kuhamasisha matumizi ya nishati iliyo safi na salama. Tunapaswa kuwa na mkakati madhubuti wa kisera na kibajeti pamoja na kuweka mazingira wezeshi katika kutatua changamoto za upatikanaji wa nishati safi,” amesisitiza Rais.
Mpango wa Serikali ni kuhakikisha mpaka mwaka 2032 inafikia asilimia 80 hadi 90 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia.