Vyakula vinavyowafaa watoto waliofikisha mwaka mmoja

Na Lucy Samson
14 Mar 2023
Mtoto wa mwaka mmoja (miezi 12) anatakiwa kupewa milo mitatu kwa siku na asusa mbili kati ya mlo na mlo.
article
  • Ni pamoja na vyakula vyenye virutubisho na nishati.
  • Mbogamboga na  vyakula vya jamii ya kunde.

Ni furaha ya kila mzazi au mlezi kuona umri wa mtoto wake ukiongezeka huku akiwa na afya njema.

Uwepo wa magonjwa nyemelezi kama Maralia, homa ya tumbo na utapiamlo ambayo husababishwa na upungufu wa kinga mwilini na lishe duni huhatarisha maisha ya mtoto.

Je unafahamu kuwa ukuaji wa mwili wa binadamu unategemea sana lishe aliyopewa tangu akiwa mdogo?.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema afya bora ya binadamu inachangiwa na lishe sahihi aliyopewa ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya mwanzo.

“Lishe sahihi katika miaka mitatu ya kwanza ya maisha hupunguza hatari ya magonjwa sugu na vifo pamoja na kukuza ukuaji wa kawaida wa kiakili na kimwili,” inasema WHO.

Makala zilizopita tuliangazia vyakula vinavyowafaa watoto baada ya umri wa miezi sita, leo tusonge na kujifunza vyakula vinavyowafaa watoto wa mwaka mmoja mpaka miaka mitatu.

Kwa mujibu wa mwongozo wa utoaji huduma ya lishe kwa watoto wadogo ulioandaliwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), mtoto wa mwaka mmoja (miezi 12) anatakiwa kupewa milo mitatu kwa siku na asusa mbili kati ya mlo na mlo.

Asusa ni chakula chepesi anachopewa mtoto wakati akisubiri muda wa kulishwa/kula chakula kingine ufike, mfano maziwa, juisi pamoja na matunda.

Wakati mtoto anasubiri mlo wa mchana au jioni unaweza kumuandalia asusa ya ndizi, karoti na brokoli au aina nyingine ya mboga mboga.Picha|Lishe tips

Vyakula vilivyokatwa katwa au kupondwa

Mara nyingi watoto wa kuanzia mwaka mmoja huwa wameanza kuota meno hivyo ni sahihi kuanza kuwapa vyakula vilivyokatwa katwa ili wajifunze kutafuna. 

TFNC wanashauri mtoto apewe chakula kile kile ambacho kinaliwa na familia ila cha kwake apewe kwenye sahani yake maalum kikiwa kimekatwa katwa au kupondwa pondwa. 

Hapa mzazi unaweza kuandaa viazi mviringo au ndizi zenye mchuzi, wali laini (bokoboko) au ugali laini na mboga ya mchuzi.

Vyakula vyenye virutubisho na nishati kwa wingi

Boresha chakula cha mtoto kwa kuongeza vyakula vyenye virutubishi na nishati kwa wingi, kama karanga, mafuta, mbegu zinazotoa mafuta, kweme, nazi au maziwa. 

Unaweza kuanza kumpa chakula nusu bakuli kisha ukaongeza chakula na virutubisho taratibu kadiri mtoto anavyokua.

TFNC wanashauri chakula cha mtoto wa mwaka mmoja lazima kiwe kizito kinachoweza kukaa kwenye kijiko bila kumiminika kwa urahisi ili kutoa nishati na virutubishi vya kutosha.Picha|Baby food.

Mbogamboga, vyakula vya jamii ya kunde na vya asili ya wanyama

Kila mlo wa mtoto usisahau mbogamboga, vyakula vyenye asili ya kunde kama maharage, njegere, kunde, karanga, soya, njugu mawe, dengu, choroko na nyingine.

Vyakula hivi vya kunde unaweza kuvitumia kama mboga utakayoiandaa kusindikiza mlo wa mtoto wako pamoja na vyakula vyenye asili ya wanyama kama  nyama, samaki, dagaa vinavyoweza kuwa mboga pia.

Zingatia haya

Taasisi ya chakula na lishe imesema ni vyema mzazi kuzingatia mambo mbalimbali wakati wa kumpa mtoto chakula ikiwemo kuhakikisha mtoto anapata makundi yote ya chakula.

 “Chakula cha mtoto lazima kiwe na mchanganyiko wa angalau chakula kimoja kutoka kwenye makundi makuu matano  ya vyakula, mlishe mtoto mara kwa mara angalau mara tano kwa siku kutegemeana na umri wake,” umeeleza mwongozo wa TFNC.

Pamoja na hayo taasisis hiyo inashauri wazazi au walezi watumie mbinu shirikishi wakati wa kumlisha mtoto ili kumuepusha kupoteza hamu ya kula au kukataa kula.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa